Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Menejimenti ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuharakisha na kuweka wazi mchakato wa ajira 12,000 zilizotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025 jijini Dodoma.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 24.11.2025 ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika taasisi hiyo tangu alipoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 18 Novemba, 2025 kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Amesema moja ya ahadi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Utumishi wa Umma unakuwa bora katika kutekeleza majukumu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa ili kuhakikisha hili linaanza kutekelezwa aliahidi kutoa vibali vya ajira 12,000 kwa Kada ya Elimu watumishi 7,000 na Kada ya Afya, watumishi 5,000.
“Kibali cha ajira kimeshatolewa, nawashukuru kwa kuanza kufanyia kazi, ni jambo zuri, ni mategemeo yangu kuwa majawabu ya maelekezo ya Mhe. Rais tutayaona hivi karibuni, hakikisheni mnasimamia kwa ukamilifu, mchakato wote wa ajira hizi uwekwe wazi ili kuondoa dhana potofu ya kuwa kuna upendeleo katika kutoa ajira.” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Ameitaka Menejimenti hiyo kuongeza kasi ya kuratibu mchakato wa ajira “Tuangalie changamoto zinazokwamisha uharakishaji wa mchakato wa ajira ili tuweze kutatua na kuendelea na kukamilisha kwa wakati.” Ameongeza.
Pia, ameielekeza Menejimenti hiyo kuzingatia maadili katika kusimamia mchakato huo wa ajira ili kuhakikisha wanapatikana watumishi sahihi na wenye vigezo. kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, ameisisitiza Menejimenti hiyo kutoonea watumishi walio chini yao bali wawaelekeze kwa upendo. “Tusimamie maadili katika utekelezaji wa majukumu yetu, tusionee watumishi walio chini yetu, tuzingatie taratibu za utendaji kazi.” Ameongeza
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesisitiza ushirikiano toka kwa Menejimenti hiyo. “Tumekuja kujitambulisha, ninaomba ushirikiano wenu, tufanye kazi kwa pamoja, tutatue kero za wananchi kama ambayo Rais wetu anatamani iwe.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bwana Mick Kiliba akielezea majukumu ya Taasisi hiyo, amemshukuru Mhe. Waziri na Viongozi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliombatana nao kwa kuona umuhimu wa kutembelea katika Ofisi hiyo na kuwahimiza uwajibikaji kwa maslahi mapana ya taifa. Pia aliahidi kukamilisha mchakato wa ajira 12,000 kwa wakati.