Ajira Elfu 70 Wizara ya mambo ya ndani 2025
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahamod Thabit Kombo, ametangaza kuwa wizara yake imepokea maombi ya ajira kutoka kwa vijana 50,000 wenye umri kati ya miaka 20 hadi 35.
Akizungumza leo, Alhamisi Oktoba 23, 2025, katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Buza jijini Dar es Salaam, Kombo amesema ajira hizo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Sita.
“Mheshimiwa Rais, katika Ilani iliyopita uliahidi ajira milioni tano. Katika ilani ya sasa, umeongeza hadi kufikia milioni nane. Leo tumepokea mkataba wa ajira 50,000 kwa vijana wa Kitanzania watakaokwenda kufanya kazi nje ya nchi. Ajira hizi zimepatikana chini ya serikali yako inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi,” amesema Kombo.
Amefafanua kuwa ajira hizo ni sehemu ya mchango wa Tanzania katika ushirikiano wa kimataifa, huku akiwataka vijana kujiandaa kwa fursa zaidi zinazokuja.
“Vijana wengine 20,000 watapata ajira za ndani ya nchi. Utaratibu wa ajira zote – za ndani na nje – unasimamiwa na Serikali, hivyo nawahimiza vijana kujitayarisha kwa mahojiano (interview) yatakayofanyika hivi karibuni. Serikali na chama chenu vitahakikisha hamkosi nafasi,” ameongeza.
Waziri Kombo amesema ajira hizo ni ushahidi wa utekelezaji wa vitendo wa Serikali ya Rais Samia, akisisitiza kuwa ahadi zilizotolewa zinatekelezwa kwa uhalisia.
“Samia Suluhu Hassan anafanya kwa vitendo, si kwa maneno, na ushahidi ni huu wa leo. Kazi imefanyika, kilichobaki sasa ni kazi kwenu Oktoba 29,” amesema.
Imeandikwa na Faraja Masinde